Apr 7, 2013

KAMPUNI YA ALLIANCE ONE KUCHANGIA VIFAA VYA UJENZI NA MADAWATI 497 YENYE THAMANI YA MIL 28 KWA SHULE ZA TABORA, KIGOMA, MARA, KAHAMA NA RUVUMA.



Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One inajiandaa kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi na madawati 497 yenye thamani ya shilingi 28,055,000 kwa shule zilizopo Tabora, Kigoma, Kahama na Ruvuma. Hii inatokana na maombi kutoka kwa jamii ya wakulima wa tumbaku katika mikoa hiyo.
Kamati ya miradi ya maendeleo ya Jamii ya Alliance One ilikutana hivi karibuni mjini Morogoro na kuidhinisha msaada huu ikiwa ni sehemu ya namna Alliance inavyojitolea kuwajibika kwa jamii. Mradi huu unalenga kusaidia jamii zilizopo ndani ya maeneo ambayo Alliance One inaendesha shughuli zake. Sera ya kampuni kuwajibika kwa jamii inalenga kusaidia katika nyanza za elimu, afya na kutunza mazingira.
Msaada ambao Alliance one inatoa kwa jamii unaenda sambamba na juhudi za serikali katika kutoa huduma za jamii kwa watu wake.
“Tunawajibika kwa Tanzania na tunashukuru kwa msaada ambao Serikali imekuwa ikitoa kwa sekta ya tumbaku na tunaamini kwamba tunawajibika kusaidia kupunguza umaskini kwa kuchangia katika elimu, afya na kuhifadhi mazingira,” alisema Mr. Mark Mason, Mkurugenzi wa AOTTL na Mwenyekiti wa CDPC.
Shule ambazo zitafaidika na msaada huu ni Shule ya Msingi Kalunde iliyopo Tabora (madawati 110), Shule ya Msingi Imalauduki (madawati 70), Shule ya St. Francis iliyopo Tabora (mifuko 20 ya mbolea), Shule ya Msingi Mulungu iliyopo Kahama (mabati 50 na mbao 120 za kuezekea darasa moja), Shule ya msingi Lugongoni iliyopo Nguruka, Kigoma (madawati 70), Shule za Msingi Mkongo Gulioni, Mlindimila na Litete zilizopo Songea, Ruvuma (madawati 30 kila moja) na Shule ya Msingi Geitasamoi liyopo Serengeti, Mara (madawati 157).
Alliance One Tobacco Tanzania Ltd (AOTTL) yenye makao makuu yake katika Manispaa ya Morogoro, maeneo ya Kingolwira, ni kampuni tanzu ya Alliance One International (AOI) ya Marekani yenye makao makuu North Carolina. Ni moja kati ya kampuni tatu Tanzania zinazonunua tumbaku na inanunua zaidi ya kilo 35 milioni kutoka katika vyama vya msingi vya ushirika 182 vyenye wanachama wakulima wapatao 39,800 kutoka Tabora, Urambo, Kahama, Manyoni, Iringa, Kasulu, Songea na Mara.


CRDT: GPL

No comments: