Apr 21, 2013

Baraza la Amani na Usalama la AU kukutana TZ

Mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika utafanyika jijini Dar es Salaam Tanzania kuanzia kesho. Rais Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa mawaziri wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU). Mkutano huo utafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Aprili 22, ukihudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka nchi wanachama wa umoja huo. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania  kwa vyombo vya habari imesema kuwa, baraza hilo lina wajumbe 15. Wajumbe hao ni kutoka kwenye kanda tano za Umoja wa Afrika za Algeria, Angola, Cameroon, Congo Brazzaville, Ivory Coast, Djibouti, Equatorial Guinea, Gambia, Guinea, Lesotho, Misri, Msumbiji, Nigeria, Uganda na mwenyeji Tanzania. Baraza hilo litakutana chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Bernard Membe ambapo litajadili pamoja na mambo mengine hali ya kisiasa nchini Madagascar ambayo iliathiriwa vibaya na mapinduzi yaliyofanyika nchini humo Machi 2009. Mkutano huo unatarajiwa kupendekeza mikakati ya kuisaidia Madagascar kufanya uchaguzi huru na wa haki Julai mwaka huu.

No comments: