Feb 25, 2013

Watetezi kesi ya Ponda wahitimisha ushahidi

Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (Kushoto) na Katibu wake,Sheikh Mukadam Swalehe wakiwa katikati ya askari magereza kwenye majengo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.Picha na Venance Nestory. 
Na  James Magai  (email the author)

Posted  Jumatatu,Februari25  2013  saa 21:15 PM
Kwa ufupi

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Victoria Nongwa, Sheikh Ponda na Sheikh Swalehe pia wanakabiliwa na tuhuma za

UPANDE wa utetezi katika kesi inayohusu tuhuma za wizi na uchochezi wa kusababisha uvunjifu wa amani, inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na mwenzake 49, umemaliza kutoa ushahidi wake.


Kesi hiyo sasa inaingia katika mchakato utakaoruhusu pande mbili za mawakili, kutoa hoja na kuzijadili ili mahakama iweze kuamua kama Ponda na wenzake wana kesi ya kujibu au la.
Sheik Ponda, kiongozi mwingine wa taasisi hiyo, Sheikh Mukadamu Swaleh na wenzao 48 wanakabiliwa na kesi ya kupora na kujimilikisha isivyo halali eneo la ardhi katika kiwanja cha Chang’ombe Markaz.

Hali kadhaliwa wanakabiliwa na tuhuma za wizi wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh59.6 milioni.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Victoria Nongwa, Sheikh Ponda na Sheikh Swalehe pia wanakabiliwa na tuhuma za uchochezi.

Hata hivyo jana upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake baada ya kuwaita mahakamani jumla ya mashahidi 17 na kuwasilisha vielelezo 13 vya ushahidi .

Wakili wa Serikali Mwandamizi (SSA) Tumaini Kweka, alitoa taarifa hiyo baada ya shahidi wa 17 wa upande wa mashtaka , Ditektivu Koplo Ismail Abdul wa Kituo cha Polisi Chang’ombe, kumaliza kutoa ushahidi wake.

Baada ya taarifa hiyo ya Jamhuri, mmoja wa mawakili wanaowatetea washtakiwa, Juma Nassoro alidai kuwa kulingana na mtiririko wa ushahidi wa upande wa mashtaka washtakiwa wote hawana kesi ya kujibu.

Baada ya majadiliano ya pande zote, Hakimu Nongwa aliamuru upande wa utetezi uwasilishe majumuisho ya hoja kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la hapo kesho na upande wa mashtaka kujibu hoja hizo.

Katika ushahidi wake, shahidi huyo wa 17, alidai kuwa aliandika maelezo ya mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo aliyemtaja kwa jina la Faisal, wakati washtakiwa hao wakiwa katika Kituo cha Polisi Kijitonyama walikokuwa wamehifadhiwa baada ya kukamatwa.

Shahidi huyo alidai kuwa katika mahojiano hayo mshtakiwa alimweleza kuwa yeye ni mkazi wa Mlandizi na kwamba alifika katika eneo la tukio alikokamatwa na wenzake baada ya kusikia tangazo katika Redio Iman inayomilikiwa na Waislam.

No comments: