Baada ya kifo cha Padre Evarist
Mushi ambae alifariki kwa kupigwa risasi Zanzibar jumapili iliyopita,
kanisa Katoliki limewataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania wengine
kuwa watulivu na kufanya maombi ya amani katika kipindi hiki.
Askofu mkuu wa kanisa hilo
Tanzania Muadhama Polycarp Cardinal Pengo amesema kifo cha Padre Mushi
ni pigo kwa kanisa na Taifa na ni ishara ya kutoweka kwa amani hivyo
hilo swala linatakiwa kufanyiwa kazi kabla ya madhara kuzidi, kwa sababu
ukikosekana usalama kwa imani moja, kesho na kesho kutwa haijulikani ni
imani gani ikashambuliwa.
Namkariri akisema “vyombo vya
usalama vinatakiwa viwe makini, mimi sio mtaalamu wa usalama lakini
naona ni jambo ambalo lingeweza kuzuilika na lisitokee kama watu
wangesoma ishara za nyakati, wale wanaohusika wazuie kisitokee chochote…
kuendeleza moyo wa kisasi hakutasaidia chochote na badala yake kutaleta
madhara zaidi”
Padre Evarist Mushi atazikwa
february 20 2013 huko Zanzibar ambapo pia misa kubwa ya kuomba amani
imepangwa kufanyika siku hiyohiyo kwenye kanisa la Mtakatifu Joseph
jijini Dar es salaam.
Kwenye sentensi nyingine ni
kwamba Serikali ya Mapinduzi Znz imewaondoa hofu wananchi wake kuhusu
ujio wa makachero kutoka nje ya nchi kwani umelenga kuliangamiza kundi
lenye mtandao wa kihalifu linalotishia amani ya Zanzibar na Tanzania.
Waziri wa nchi ofisi ya makamu
wa pili wa Rais Zanzibar Mohamed Aboud amesema Serikali imekerwa na
matukio ya kushambuliwa kwa viongozi wa dini, matukio ambayo yanaendelea
kutokea ndio maana inaamini uamuzi wa kuwatumia makachero kutoka nje ya
Tanzania utasaidia kuumaliza mtandao unaofanya uhalifu huo.
Namkariri akisema “Wenzetu hawa
wa mataifa makubwa wameendelea sana na wamefanya mambo haya kwa muda
mrefu, inastaajabisha sana kwa mtu wa Zanzibar kutokea akaenda kumpinga
risasi mtu asie na hatia, haijawahi kutokea mtindo huu”
Askofu wa kanisa katoliki Znz
Agostino Shao amesema “kuna watu ambao wamepandikizwa tayari na wanakuja
kwa mwamvuli wa dini ya kiislam, sasa hao ndio wanaharibu Uislamu wetu
na hao wengine ndio wanaoharibu dini yetu ya kikristo pia, sidhani kama
haya yanayofanyika Znz yameundiwa hapahapa kwa sababu ukimuuliza
Mzanzibar yeyote hata Rais anasema mimi nimesoma Mission, karibu wote
wamesoma shule za Mission… “
Kwenye mstari mwingine Askofu
Shao amesema “hii ni shida inayopandikizwa na watu wenye njia mbaya
maana ukishasema Waislamu unamjumuisha na hata mama mzee, kibibi
kilichoishi kwa miaka yote hiyo Uislamu wake mzuri, Wazee wetu wameishi
Uislamu wao mzuri wakichanganyika na wengine leo ndio mnasema ndio
analete fujo hataki kuishi na Wakristo, mimi nisingependa kusema ni
Waislamu wote kwa ujumla wanahusika, katika kila dini kuna watu wazuri
na Waovu, baadhi ya Waislamu ambao wana sera zao za tofauti na dini hii
ya Kiislam ndio wanaweza kuwa watendaji, baadhi ya Wakristo ambao wana
siri zao za dini yao ndio wanaweza kuwa watendaji, lakini ukisema
Waislamu wote nitakataa”
No comments:
Post a Comment