Jan 15, 2011

Masanja atia aibu ukumbini!!!!!!


Mchekeshaji ‘brazameni’ wa Kundi la Orijino Komedi linalovunja mawingu kupitia kituo cha Runinga cha TBC1, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ (pichani) ametia aibu na zigo lote kubebeshwa kwa mke atakayemuoa.

Masanja alishuhudiwa akifakamia msosi kwa kubeba sahani mbili kwa mpigo tofauti na utaratibu na watu wengine.

Tukio hilo la aibu lilijiri ndani ya Ukumbi wa Mzalendo Pub Millennium Towers, Kijitonyama, Dar es Salaaam usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii ambapo Bendi ya African Stars International ‘Twanga Pepeta’ ilikuwa imeandaa sherehe maalum ya mastaa wa Bongo iliyokwenda kwa jina la ‘Celebrity Party’.

Stori nzima ilikuwa hivi; Akiwa miongoni mwa mastaa waalikwa, Masanja aligeuka kituko baada ya kupiga watu vikumbo katika meza ya msosi kisha kubeba chakula sahani mbili na kuanza kuzifukia kama mtu aliyekuwa anakimbizwa.

Baada ya Paparazi wa Risasi Jumamosi kuona kituko hicho, king’ora kiligonga kuashiria kuwa staa huyo anafaa kutengeneza kichwa cha habari kwa kuwa siyo jambo la kawaida katika malezi ya jamii ya watu waliostaarabika, hivyo ‘kumfotoa’ picha za ushahidi.

Tukio hilo liliwashangaza baadhi ya mastaa ukumbini humo ambao walikuwa wakimkodolea macho huku wakinong’ona kuwa hata mke atakayemuoa atakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha jamaa anashiba.

Baada ya Masanja kumaliza ‘kubugia’, Paparazi wetu ambaye alikuwa akimfuatilia hatua kwa hatua alimfuata ili kujua kulikoni ‘kucheza rafu’ kwenye msosi ambapo jamaa alitaka ishu hiyo ‘ichuniwe’.

“Isiwe ishu, mwanangu ichunie,” alisema Masanja. 
Siyo mara ya kwanza kwa staa huyo kufanya tukio la aina hiyo kwani aliwahi kuripotiwa na gazeti tumbo moja na hili, Risasi Mchanganyiko ambapo alinaswa akifanya hivyo kwenye sherehe ya kuhitimu chuo kikuu ya mcheza filamu za Kibongo, Emmanuel Myamba iliyofanyika katika Ukumbi wa Makete, Mbezi Beach, Dar.

No comments: