Jan 6, 2011

Kilichotokea Kwenye Maandamano Arusha!

Ndugu Zangu,JUMA lililopita Watanzania, na dunia pia, tuliona kupitia televisheni na vyombo vingine vya habari, picha zikiwaonyesha polisi wetu wakipambana na waandamanaji wafuasi wa Chama Cha Wananchi, CUF. Ilisikitisha sana.
Pengine polisi ‘kupambana’ na waandamanaji si neno sahihi. Mara nyingi tunachokiona ni polisi ’kuwaandama’ waandamanaji. Hii ni pamoja na polisi kuwatawanya waandamanaji kwa virungu, mabomu ya machozi, risasi za mipira na hata za moto.
Jana tena, Watanzania na dunia, tumeona picha za televisheni zikiwaonyesha polisi wetu wakipambana ama kuwaandama waandamanaji wafuasi wa CHADEMA kule Arusha . Imeripotiwa na BBC kuwa kuna Watanzania waliopoteza maisha. Inasikitisha sana. Na unapoangalia picha hizi zenye kuharibu taswira njema ya nchi yetu ndani na nje ya mipaka yetu unajiuliza; KWANINI?



Kwa watawala Afrika, hakuna msamiati wa ’ Maandamano’ , kuna ’ MATEMBEZI ya MSHIKAMANO’. Afrika hakuna dhambi ya kuandamana kuunga mkono au kupongeza kauli au jambo lililotendwa na upande wa utawala. Dhambi ni kuandamana kupinga. Tujiulize tena; nini maana ya maandamano?

Tunaamini katika demokrasia, maandamano ni namna pia ya kujieleza. Muhimu katika maandamano ni kuhakikisha kuwa yanakuwa ni ya amani na utulivu. Wenye kuandamana waandamane na wengine waendelee na shughuli zao. Na hapa ni jukumu la wenye kuandaa maandamano kwa kuwashirikisha polisi.

Kuwepo na utaratibu unaoeleweka. Wapi waandamanaji watakusanyikia kabla ya kuanza maandamano. Hivyo basi, wapi maandamano yataanzia, umbali wa kilomita ngapi, kwa kupita barabara zipi na wapi yataishia. Hayo yanaweza kufanyika kwa ustaarabu kabisa.

Jukumu la polisi litakuwa ni kuyaongoza na kuhakikisha hakuna vurugu zinazotoka miongoni mwa waandamanaji, na si kinyume chake. Kwanini kuwepo na hofu ya vurugu wakati wenye kuandamana ni wafuasi wa chama au kikundi kimoja cha kijamii kwa wakati mmoja, tena wakiwa na viongozi wao?

Mchumba wa DK. Slaa, Bi. JosephineDunia imebadilika, tunahitaji kubadilika pia. Jeshi letu la polisi lijipange upya. Kwa jinsi picha za televisheni zinavyoonyesha polisi wetu wanavyowapiga virungu na hata kuwarushia risasi waandamanaji wasio na silaha inaamsha hisia mbaya kwa Watanzania. Inaleta taswira mbaya ya nchi yetu kwa jumuiya ya kimataifa. Inasikitisha sana. Ni aibu kwa nchi yetu tuliyozaliwa na tunayoipenda sana. Tubadilike.

No comments: