Jun 6, 2013

TUSIPOCHUKUA HATUA, DAWA ZA KULEVYA ZITAWAMALIZA WANAMICHEZO NA WANAMUZIKI WA TANZANIA

DAWA za kulevya ni hatari, ni hatari sana. Maisha ya baadhi ya wasanii na wachezaji yamepotea kutokana na matumizi ya dawa hizo.

Aidha, dawa za kulevya husababisha baadhi ya wasanii na wachezaji kushindwa kuendelea na fani zao.
Orodha ya wasanii waliopoteza maisha kutokana na matumizi ya dawa za kulevya ni ndefu lakini baadhi yao ni Elvis Presley, Whitney Houston, Brenda Fassie wa Afrika Kusini.

Tanzania imepata mshtuko kwamba kimeripotiwa kifo cha msanii kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. Tukiwa tunangoja ripoti kamili ya daktari juu ya kifo chake, msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya ‘Bongo Fleva’, Albert Mangwea ‘Mangwair au Ngwea’ anadaiwa kufariki kutokana na dawa za kulevya nchini Afrika Kusini mapema wiki iliyopita.

Habari hizo ziwe kweli au la, Mangwair amefariki na mwili wake ulirejeshwa nchini juzi kwa mazishi yaliyofanyika jana huko Morogoro. Hata hivyo kifo chake, kitoe changamoto kwa wasanii wengine 
akiwemo Ray C aliyeko kwenye kituo cha kujirekebisha kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.



DAWA ZA KULEVYA
Hizi ni dawa ambazo zimepigwa marufuku kutumiwa na jamii kutokana na kiwango chake cha athari kwa binadamu. Dawa hizi ambazo miongoni mwake ni bangi, heroin na cocaine, zina athari zaidi katika mwili wa binadamu kuliko faida.

Wasanii wanaotumia dawa za kulevya husukumwa zaidi na tabia ya kuiga ili waweze kufanya maonyesho jukwaani kwa ukakamavu mkubwa.

Wasanii hawa wanaamini wanapotumia dawa hizo zinawasisimua mwili ili wapate uwezo wa kutumbuiza jukwaani kwa muda mrefu bila kuchoka tena bila aibu.

Upande wa wanamichezo hasa soka na riadha, msukumo mkubwa upo katika kuwa na pumzi ya kuweza kucheza soka kwa dakika 90 bila kuchoka na moyo wa ujasiri hata kwenye riadha hali ni hivyo hivyo.

ATHARI ZA DAWA ZA KULEVYA MICHEZONI

Serikali duniani kote zinapiga marufuku matumizi ya dawa za kulevya. Kwa bahati mbaya, dawa hizi hutengenezwa, husafirishwa na hutumiwa kwa kificho japokuwa madhara hujionyesha wazi.

Kwa mujibu wa wataalam, mtu anapotumia dawa za kulevya, moja kwa moja huathiri baadhi ya viungo vya mwili kinyume cha imani ya watumiaji.

Mtumiaji hupata ganzi na kutoka katika hali ya kawaida. Kutokana na ganzi hiyo taarifa hutumwa katika ubongo na ubongo nao hutuma vichocheo katika kiungo hicho na hufanya kazi maradufu.

Jinsi dawa inavyotumiwa kwa wingi ili kurekebisha hali ya ganzi ndivyo nguvu inavyozidi kutengenezwa na hivyo ndivyo vinavyowamaliza wasanii na wanamichezo.

Wataalam wanasema matumizi haya ya dawa za kulevya huufanya mwili wa mtumiaji kuchoka na kukosa hamu ya kula kutokana na seli nyingi mwilini kushindwa kufanya kazi.

Matokeo yake, mwili wa mtu huyo hudhoofu kwa kukosa chakula na hata uwezo wa kutengeneza chembechembe hai za kuulinda mwili na kujikinga dhidi ya magonjwa hupungua, hivyo mwili huruhusu magonjwa ya mara kwa mara.

Hali hii inapotokea uwezo wa msanii au mwanamichezo huonekana umepungua na muda wowote mahala popote anaweza kuchukua maamuzi anayoyajua yeye.

KITU CHA KUFANYA

Masomo ya dini za Kikristo na Kiislamu na elimu maalum ya dawa za kulevya yatumike ili kuwaweka vijana katika misingi mizuri ya maadili na athari za dawa za kulevya.

Hii itasaidia vijana kufahamu kwa undani faida za dawa zilizoidhinishwa na Serikali na athari za dawa zilizopigwa marufuku zikiwemo za kulevya ili kupunguza kwa wimbi la vijana kutumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya.

MAKALA HII IMETOLEWA KATIKA GAZETI LA MAWIO NA IMEANDIKWA NA ELIUS KAMBILI

                                              SOURCE: MPEKUZI BLOG

No comments: