Jun 27, 2013

"TUNAMTAKA WAZIRI MKUU PINDA AOMBE RADHI WATANZANIA, AKIKATAA BASI AWAJIBISHWE KWA MUJIBU WA SHERIA"...HAKI ZA BINADAMU

Akizungumza na waandishi wa habari jana  Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo-Bisimba amesema kitendo cha Waziri Mkuu Bizengo Pinda kuruhusu matumizi ya nguvu kwa polisi dhidi ya raia ni cha kulaaniwa na wapenda haki wote na amemtaka waziri mkuu kuwaomba radhi watanzania. KUPINGA KAULI YA WAZIRI MKUU "Wapigwe tu" ALIYOITOA BUNGENI TAREHE 20/06/2013

Taarifa hii ni matokeo ya ufuatiliaji wa utendaji wa shughuli za Serikali kama zinavyowasilishwa bungeni na kauli ya Waziri Mkuu (Mtendaji Mkuu wa shughuli za serikali Bungeni) aliyoitoa, Alhamisi ya tarehe 20 Juni 2013, wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo. 

Waziri Mkuu Pinda, alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama, hususan Jeshi la Polisi kuwapiga wananchi watakao kaidi na kupinga amri halali ya jeshi hilo. Katika tamko hilo, Pinda alisema Serikali imechoshwa na vurugu na kwamba hakuna namna nyingine ya kupambana na wananchi wanaodharau vyombo vya dola zaidi ya kipigo.

Waziri Mkuu Pinda alitoa msimamo huo Bungeni, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kufuatia kuwa na matukio ya vurugu ya mara kwa mara nchini, hususan huko Mtwara na Arusha.
Katika majibu yake, Mh. Pinda, pamoja na mambo mengine alisema kuwa; “Mheshimiwa Mangungu hapa ameanza vizuri, lakini mwisho hapa naona anasema vyombo vya dola vinapiga watu, ukifanya fujo au umeambiwa usifanye hiki ukaamua kukaidi utapigwa tu. 

Akaendelea kusema kuwa, “Lazima wote tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya sheria na kama wewe umekaidi, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi, watakupiga tu.

“Na mimi nasema wanaokaidi amri halali ya Jeshi la Polisi muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine ya kupambana na wakaidi zaidi ya kuwapiga,alisema Pinda.

Ndugu wanahabari, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimepokea kwa mshituko kauli hii iliyotolewa na kiongozi wa juu serikalini. Maudhui ya kauli hii ni kinyume kabisa cha Katiba ,Sheria za nchi na misingi ya haki za binadamu.

 katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu hasa yale yanayotokana na vyombo vya dola na jeshi la polisi nchini, ambapo jeshi la polisi limekuwa likitumia nguvu kubwa kupita kiasi katika matukio mbali mbali na kusababisha vifo na kujeruhi watu na hata watu ambao hawakukiuka amri halali ya jeshi hilo.

Matukio haya ya matumizi makubwa ya nguvu za dola ni kinyume na taratibu za utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 13 (1) Usawa mbele ya sheria , (3)” Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na Mahakama na vyombo vingine vya mamlaka ya nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria” na (6) (b) ambayo inasema ni “Ni marufuku kwa mtu ………….kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka atakapo thibitika kuwa anayohatia ya kutenda kosa hilo” (e) Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazo mtweza au kumdhalilisha.”

Pia ni Kinyume na kifungu namba 21 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inayounda sura namba 20 ya sheria za Tanzania inayozuia matumizi ya nguvu kupita kiasi na kifungu namba 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma saidizi “Police force and auxiliary Act” Sura namba 322 kama zilivyorekebishwa mwaka 2002, ambayo inaelekeza kukamatwa kwa mtu aliyetenda kosa na si kupigwa. 

Matumizi makubwa ya nguvu pia ni kinyume na Mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na Tanzania na inayotambuliwa kwenye Katiba kama Tamko la Haki za Binadamu la Mwaka 1948 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa Mwaka 1966.

Tungependa kumkumbusha mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa Utawala wa sheria unajumuisha serikali, na vyombo vya utekelezaji na ulinzi pamoja na wananchi kuheshimu sheria. Na sio kuvunja sheria kwa vyombo vya usimamizi wa sheria. Tamko hili la Waziri Mkuu limetoa mwanya mkubwa na a nguvu kwa vyombo vya usimamizi wa sheria kuvunja haki za raia. 

Ikumbwe kuwa yapo matukio mengi ya polisi kutumia vibaya nafasi yao na nguvu waliyonayo katika kuwavunjia haki wananchi kama mauaji yaliyofanywa huko Songea mwezi wa Pili mwaka 2012 ambapo watu wawili waliuwawa na polisi na wengine 48 kujeruhiwa, Iringa mwezi wa tisa 2012 ambapo mtu mmoja aliuwawa (Daudi Mwangosya), Tabora - Usinge 2011 ambapo mtu mmoja aliuwawa. 

Haya ni baadhi tu ya matokeo ya matumizi makubwa ya nguvu ya polisi. Pamoja na hayo yapo matukio ya polisi kuuwa raia na kuwajeruhi kwenye matukio tofauti tofauti hapa nchini ambayo mpaka sasa Kituo kina matukio ya watu 11 ambao wameuwawa mikononi mwa polisi. Haya yote yanatokea kwa sababu jeshi la polisi limeshindwa kufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria na pia kutambua wajibu wao kwa wananchi.

Katika hali hii ya kushtusha, kwenye nchi yenye Amani na Utulivu na kama tunavyopenda kusema kisiwa cha amani, kiongozi huyu wa ngazi za juu anatoa tamko linaloashiria kutoa ruksa kwa Jeshi la polisi kuvunja sheria tena tamko linatolewa hadharani, mbele ya chombo kinachoheshimika kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tofauti na misingi ya Katiba na Haki za Binadamu ni hatari kwa amani na utulivi huo. .

 Waziri Mkuu anapaswa kuheshimu na kuilinda katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za nchi na kuhakikisha usalama wa raia.

Hivyo basi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Watanzania wanaopenda heshima ya sheria na haki za binadamu na asasi za kiraia tumeendaa waraka unaokusanya saini za watanzania zikimtaka Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda;

1. Kwanza kabisa kufuta kauli yake aliyoitoa bungeni kubariki polisi kupiga raia katika Mkutano huu wa Bunge la Bajeti.

2. Kuwaomba radhi Watanzania kwa kile alichosema bungeni.

3. Kulielekeza jeshi la polisi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizoko katika kutekeleza kazi zake za kulinda usalama wa raia na mali zao.

Mpaka sasa tumeshakusanya saini 1000 kudai kauli hii ifutwe ilikulinda maisha ya Watanzania.

No comments: