Jun 16, 2013

MKASA MZIMA KUHUSU KUPIGWA KWA MBUNGE NASSARI KATIKA KITUO CHA KURA MAKUYUNI


Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari ameshambuliwa na vijana wa Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Kiongozi wa Chama cha Mapinduzi, Mkoa wa Arusha aliyejulikana kwa jina la Kalanga na  kulazimika kulazwa katika hopitali ya Selian Mkoani Arusha katika fujo zilizotokea katika kituo cha kupigia kura cha Zaburi, kata ya Makuyuni, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.

Akizungumza kutoka eneo la tukio, Mratibu wa wanawake wa Chadema Mkoa wa Arusha Sesilia Ndossi alisema “muda wa saa 5 asubuhi tulienda katika kituo cha kupiga kura cha Zaburi, kumsindikiza Mbunge wa Arumeru ambaye katika Uchaguzi huo yeye alikuwa Wakala.

"Lakini tulipofika hapo tulimkuta raia mmoja mwenye asili ya kisomali akiwaita watu na kuwaambia pigia CCM, ndipo Nassari akamuuliza kwanini unapiga kampeni kituoni...

"Huyo Baba alihamaki, akamrukia Nassari wakamchangia na Diwani mmoja aliyeitwa Kalanga, wakamsukuma akaanguka damu ikaanza kumtoka puani...

"Baada ya hapo,tukalazimika kuingilia kati na kuondoka na Nassari akaenda mahali tulipokuwa tunalala akabadili mavazi akaenda kutibiwa Minjingu,  


"Hata tulipofika huko waliendelea kutufuata wakaja na gari imejaa vijana wa kimasai wakimtafuta Nassari. Tulivyoona  hivyo, tulilazimika kukodi gari ambayo hawaifahamu ndipo tukamwondoa kumpeleka Arusha hospitali ya Selian kwa matibabu zaidi."

Taarifa zaidi kutoka Makuyuni zinasema walipomkosa Nassari walimpiga dereva wake Gadi Palangyo  na Katibu wa Chadema wa Wilaya ya Monduli, Thomas Kilongola, hadi walipokuja kuokolewa na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Makuyuni. 

Hadi tunaandika habari hii Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas hakupatikana kuzungumzia suala hili baada ya simu yake kuita bila mafanikio.

No comments: