MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Dodoma Mjini, jana ilimuachia huru Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (41), maarufu kama Sugu aliyefikishwa mahakamani kwa kosa la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda baada ya hati ya mashtaka kuonesha mapungufu.
Kutokana na uamuzi huo wa Mahakama imeutaka upande wa mashtaka
kurekebisha hati hiyo na kumfikisha tena mshtakiwa mahakamani huku
Wakili wa Mbilinyi, Tundu Lissu akitaka kesi mpya itakayoletwa
mahakamani iwe na maelezo ya Waziri Mkuu na awe tayari kusimama
mahakamani kuthibitisha shitaka hilo.
Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Elinaza Luvanda.
Awali akimsomea mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Harriet
Lopa alidai kuwa Juni 24, mwaka huu, Mbilinyi akiwa Dodoma alituma
ujumbe wenye lugha ya matusi kwa kutumia mtandao wa kijamii wa Facebook
kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Mshtakiwa alikana shitaka hilo. Hata hivyo wakili wa Mshtakiwa, Lissu
aliomba kutoa hoja na kusema hati ya mashtaka ni mbovu na kuomba
Mahakama itupilie mbali kwa sababu ina makosa.
“Lugha ya matusi haikutajwa, lugha gani hiyo ya matusi na hati ya
mashtaka iko kimya, mshtakiwa atajitetea vipi,ataandaa utetezi namna
gani kwani hata kinachodaiwa kuwekwa kwenye facebook hakijasemwa,”
alidai Lissu.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali alisema kesi hiyo bado iko
kwenye upelelezi na kutaka mshtakiwa aendelee na mashtaka yake mpaka
itakapothibitishwa vinginevyo.
Kutokana na kauli hiyo ya wakili wa Serikali, Lissu alizidi
kusisitiza hati ya mashtaka haina maelezo ya kutosha na inatakiwa
kukidhi matakwa ya sheria.
“Hati ya mashtaka iliyoletwa si halali kinyume na kifungu cha 132 cha
mwenendo wa makosa ya jinai na itakuwa makosa kama Mahakama ikikubali
hati hiyo,” alisema.
Alitoa uamuzi wa Mahakama, Hakimu Luvanda alisema anakubaliana na
maelezo ya Wakili upande wa utetezi Lissu kuwa hati hiyo ina mapungufu.
Alisema Mahakama inamuachia huru mshtakiwa na upande wa mashtaka
unaweza kumshtaki tena mshtakiwa kama itaona umuhimu wa kufanya hivyo.
Akizungumza nje ya Mahakama Lissu alisema hati ya mashtaka dhidi ya
Mbilinyi kuwa alitoa lugha ya matusi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda
haijaeleza anachodaiwa kusema Mbilinyi.
Alisema Mahakama imetenda sawasawa kuifuta hati hiyo ilitakiwa
ifafanue lugha ya matusi iliyotumika ni ipi. ”Hakimu hajasema Sugu hana
makosa, lakini upande wa mashtaka ukajipange kutengeneza hati mpya,”
alisema.
No comments:
Post a Comment