Mar 15, 2013

HILI NDIO LILE SAKATA LA MWANAMKE ALIYECHINJWA KAMA KUKU NA MPENZI WAKE HUKO KAHAMA

VILIO vilitawala Kata ya Nyahanga wilayani hapa wakati wa kuuaga mwili wa binti Jessica Elialinga (19) aliyeuawa kinyama kwa kuchinjwa kama kuku na mpenzi wake, Musa Petro (27) mkazi wa Shunu kwa sababu zinazodaiwa ni wivu wa kimapenzi.


Jessica Elialinga baada ya kuchinjwa.
Tukio hilo lililoibua simanzi kubwa kutokana na marehemu kuhitimu Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Nyihogo, Kahama mwaka jana, lilijiri saa 12:45 Februari 6, mwaka huu.

Kitendo hicho kilifanyika katika banda la mbuzi lililopo nyumbani kwa kijana huyo ambaye baada ya kutekeleza mauaji na yeye alifanya jaribio la kutaka kujitoa roho kwa kisu.

Akisimulia juu ya tukio hilo, rafiki wa karibu wa Musa ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa ajili ya usalama, alisema wiki moja kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa huyo alikuwa akiwatangazia jamaa zake kwamba ana dhamira ya kumuua binti huyo kufuatia kubaini kuwa anamsaliti kimapenzi.

Muuaji Musa Petro.
 “Unajua Musa anafanya kazi ya kuchuna ngozi za wanyama machinjio ya Wilaya ya Kahama, alitutangazia dhamira yake hiyo, lakini tulichukulia kauli yake kama mzaha.

“Alisema anataka kufanya hivyo kwa sababu amekuwa akitumia gharama kubwa kwa mpenzi wake huyo tangu walipoanza uhusiano, msichana akiwa kidato cha pili, lakini anatoka kimapenzi na mwanaume mwingine,” alisema rafiki huyo.

 Hata hivyo, inadaiwa baada ya mtafaruku wa usaliti, wawili hao walipatana na kuendelea na mapenzi, lakini baada ya mwanafunzi huyo kuhitimu kidato cha nne alibadilika ambapo mwanaume alisikia kuwa tayari ana mwanaume mwingine kutoka jijini Mwanza ambaye walikubaliana kufunga pingu za maisha baada ya kumaliza masomo.

Jessica Elialinga enzi za uhai wake.
 Inadaiwa siku chache kabla ya mauaji hayo, rafiki mmoja wa karibu wa mtuhumiwa alikutana na marehemu njiani na kumsimamisha kwa lengo la kumweleza kauli zenye kutishia maisha yake anazozitoa mpenzi wake, lakini binti huyo hakusimama kumsikiliza.

 Baada ya Musa kudaiwa kufaulu kumchinja mpenzi wake huyo na yeye kujikata koromeo na kuanguka akiwa ameishiwa nguvu, kijana mchunga mbuzi ambaye wengi katika eneo hilo humchukulia kama kaka yake Jessica, ndiye aliyekuwa wa kwanza kumshuhudia Musa akiwa katika hali hiyo.

Alipomhoji kulikoni, hakupata jibu zaidi ya kushuhudia jitihada za mtuhumiwa huyo kufungua mlango wa chumbani mwake zikishindikana.
Kijana huyo alitoa taarifa kwa watu ambao walifika na kumchukua Musa na kumkimbiza hospitali ya wilaya kuokoa uhai wake.

Watu waliobaki nyumbani walifuatilia michirizi ya damu hadi kwenye zizi la mbuzi ambako walimkuta Jessica ameshafariki dunia baada ya kuchinjwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Everest Mangala alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Kahama katika Hospitali ya wilaya hiyo anakoendelea kupatiwa matibabu.

No comments: