Feb 25, 2013

SERIKALI YA AWAMU YA NNE YAONGOZA KWA KUKOPA



TAASISI isiyo ya kiserikali ina yojishughulisha na masuala ya Madeni ya Taifa na Maendeleo (TCDD), imesema Serikali ya Tanzania ndiyo inaongoza kwa kukopa zaidi, ikieleza kuwa kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2011, imekopa kiasi cha Sh15trilioni na kufanya deni la taifa kufikia Sh21trilioni.

Rais Kikwete aliingia madarakani mwaka 2005, baada ya rais aliye mtangulia, Benjamin Mkapa kumaliza kipindi chake cha uongozi wa miaka 10 kilichoanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005.

TCDD imebainisha kuwa Serikali inakopa fedha hizo kutoka Benki Kuu (BoT), Benki za Biashara, Kampuni za Bima na Mashirika ya Hifadhi za Jamii. Pia inakopa katika taasisi za kimataifa ikiwamo, Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Katika maelezo yake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Hebron Mwakagenda, alisema kuwa kite ndo cha Serikali kukopa fedha kwa ajili ya matumizi yasiyo muhimu pamoja na kuwalipa watumishi wake mishahara, ndiyo sababu ya kukua kwa deni hilo la taifa.

“Serikali ya awamu ya nne imekopa kwa kiwango kikubwa, kwani tangu iingie madarakani imeshakopa Sh15trilioni, sasa sijui mpaka inamaliza muda wake itakuwa imekopa kiasi gani?” alisema Mwakagenda akihoji na kuongeza;

“Hata kama kukopa ni kuzuri basi tukope na fedha tuzifanyie mambo ya maana hasa katika maendeleo, tukope tu pale inapokuwa lazima kufanya hivyo.”

TCDD imeeleza kwamba hali hiyo ni hatari, hasa ikizingatiwa kuwa miaka kadhaa iliyopita, Tanzania kupitia Mpango wa Nchi Maskini zenye Madeni Makubwa (HIPC), ilifutiwa kiasi kikubwa cha madeni, lakini sasa imeanza kukopa tena na deni kukua kwa kasi.

Taasisi hiyo pia imesema kitendo hicho kimechangia kuporomoka kwa uchumi wa taifa kunakosababishwa na riba kubwa za mikopo hiyo, ambapo kulingana na idadi ya Watanzania ukigawanya deni hilo kwa wote, inaonyesha kuwa kila Mtanzania anadaiwa wastani wa Sh450,000.

Mwakagenda, ambaye taasisi yake inafanya kazi ya kuishauri Serikali katika suala zima la deni la taifa na maendeleo, alisema hadi kufikia Oktoba mwaka jana, deni la nje lilikuwa Sh15.9 trilioni.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyoitoa bungeni mjini Dodoma mwaka jana, taifa linapoteza Sh3 trilioni katika ukwepaji wa kodi na ubadhirifu, huku akishauri kuwa mambo mawili yakifanyiwa kazi deni hilo litapungua au kumalizika kabisa.

“Deni linakuwa kwa kiasi kikubwa na tunakopa katika mabenki ya biashara, ambayo riba yake ni kubwa, fedha nyingi zinazokopwa hutumika kulipa mishahara,” alisema Mwakagenda.

Alifafanua kwamba mwaka 2007 hadi 2008 deni la taifa lilikuwa Sh6.4 trilioni na kwamba, kuanzia mwaka 2007 hadi 2011 deni hilo limeongezeka hadi Sh21 trilioni.

No comments: