MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto ameitaka Serikali kutoipatia leseni ya uchimbaji wa madini ya urani, kampuni ya Uhuru One hadi iilipe Serikali kodi ya Sh297 bilioni.
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alitoa pendekezo hilo bungeni mjini Dodoma jana aliposimama na kutumia kanuni ya 68(1) kueleza kutoridhishwa na majibu ya Serikali kwenye swali la 353.
Katika swali hilo, Mbunge wa Jimbo la Mkoani, Ali Khamis Seif (CUF), alitaka kufahamu Serikali itanufaika vipi na uchimbaji wa urani utakaoanza mwakani katika hifadhi ya Selous.
Katika majibu yake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema uchimbaji wa madini hayo utailipa Serikali
mrabaha wa asilimia tano ya urani yote itakayozalishwa.
Pia alisema Serikali itashiriki katika miradi ya urani kwa kuwa na hisa bila kuwekeza mtaji wowote na kupata gawio kama mwana hisa,
achilia mbali kodi mbalimbali itakazolipwa.
Hata hivyo, Zitto alisema baada ya Kampuni ya Mantra ya Australia kukamilisha kazi ya utafiti wa urani, iliuzwa kwa kampuni ya Urusi
inayojulikana kama ARZM kwa Dola za Marekani 980 milioni.
Alisema baada ya mauzo hayo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) , walitaka walipwe asilimia 20 kama kodi ambayo ni Dola 186 milioni za Marekani, sawa na Sh297 bilioni.
“Uhuru One inayotaka kuchimba madini hayo ya Urani ni kampuni tanzu ya ARZM ya Urusi tutasikitika sana kama leseni ya uchimbaji itatolewa kabla ya kulipwa kwa kodi hiyo,” alisema.
Hata hivyo, katika maelezo yake hayo, Zitto hakufafanua sababu za fedha hizo kutolipwa hadi sasa lakini alisisitiza kuwa ni vyema
Serikali isitoe leseni ya uchimbaji hadi zilipwe.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema, Serikali inafahamu zaidi kuhusu jambo hilo na kwamba
leseni haijatolewa na haitatolewa.
No comments:
Post a Comment