
Na Lost-9fm
Ile fainali ya kumpata Mkali wa Kuchekesha iliyokuwa ikisubiriwa kwa shauku kubwa na wapenzi wa sanaa ya maigizo ya kuchekesha nchini, inafanyika leo ndani ya Ukumbi wa Mango Garden Kinondoni, Dar es Salaam.
Fainali hiyo inawakutanisha wasanii watano waliochaguliwa kwa kura nyingi na wasomaji wa Magazeti ya Global Publishers na kufanikiwa kuingia hatua ya Tano Bora.
Wasanii hao ni King Majuto, Masanja, Joti, Kingwendu na Masele ambapo mshindi wa kwanza kati yao atajinyakulia kitita cha Tsh. 1,500,000/.
Mshindi wa pili ataondoka na Tsh. 1,000,000 na wa tatu atapata Tsh. 500,000 na watakaoshika nafasi ya nne na tano watapata kifuta jasho cha Tsh. 250,000.
Mgeni rasmi atakuwa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azzan na kiingilio kitakuwa shilingi 8,000/.
Bendi ya muziki wa ndansi nchini ya African Stars International ’Twanga Pepeta’, itaongoza burudani huku wasanii wa Bongo Fleva, Sam Morgan, TMK Unit, Tox Star na Ziro 4, nao watatoa burudani ya ‘kufa mtu’.
Shindano hilo lililoanza Novemba, mwaka jana, lilishirikisha wasanii 17 ambao ni Zembwela, Bi.Kiroboto, Pembe, Senga, MacRegan, Wakuvwanga, Mtanga, Mkwere, Vengu, Bambo, Mpoki na Maringo Saba.
Wengine ni King Majuto, Masanja, Joti, Kingendu na Masele ambao walifanikiwa kutinga Tano Bora na ndiyo wanachuana leo.
Shindano hilo linadhaminiwa na Allure International Model, Dar es Salaam City College - Kimara, Giraffe Hotel, Jarida la Malaika, Cream Pub- Kinondoni, Dotnata Decoration, Manywele Beauty Cosmetics na ASET Ltd.
No comments:
Post a Comment