Ndugu Zangu,
ZAMANI kwenye Radio Tanzania, moja ya vipindi maarufu kilikuwa ’ Mazungumzo Baada Ya Habari’. Ni moja ya nyenzo za Serikali kufikisha ujumbe kusudiwa kwa umma.
Ni kupitia mazungumzo yale ya dakika tano yalioandaliwa kwa umakini mkubwa, umma uliweza, mathalan, kufahamishwa ni nani adui wa umma na hitimisho la nini cha kufanywa. Hizo zilikuwa kazi za makada ’ waliokunywa maji ya bendera!’.
Unazungumzia majina kama akina Paul Sozigwa na David Wakati. Ni akina Paul Sozigwa, waliowafanya, watoto wa wakati huo, waamini , kuwa Idi Amin alikuwa aina ya nyoka!
Wakati umebadilika. Yaliyotokea Arusha ni kielelezo cha wakati uliobadilika. Siku mbili hizi, kwenye runinga na redio tunaona na kusikia kinachofanana na Mazungumzo Baada ya Habari ya enzi za akina Paul Sozigwa. Hapa wapanga mikakati wanakosea.
Tanzania ya miaka 1970 si ya 2011. Ndio maana ya umuhimu wa kubadilika na kwenda na wakati. Kwa dola, kuna wakati inahitaji kuonyesha ukali, na kuna wakati inatakiwa ionyeshe upole.
Kwa kilichotokea Arusha na jinsi Watanzania na dunia walivyoipokea habari ile ya raia wasio na silaha kuawa kwa risasi za moto na wengine kujeruhiwa, basi, dola inatakiwa kutambua mapungufu yaliyotokea. Kwa namna yake, kama alivyofanya Mh. Rais, kuonyesha masikitiko yake na kutoa matumaini ya baadae, kuwa jambo hilo laweza kuwa ni historia.
Lakini, tatizo la nchi zetu hizi ni kuongozwa na vyama dola. Hili la Arusha limefanywa kuwa siasa zaidi. Na hapa hakuna cha udini bali udini unaoingizwa na wanasiasa kwenye siasa kwa maslahi ya kisiasa.
Na kinachojitokeza sasa ni mapambano ya kutamfuta mshindi. Hapa sasa anatafutwa nani zaidi kati ya CCM na CHADEMA? Jibu ni jepesi. Hakuna aliye zaidi. Ndio, hakuna mshindi. Kwa kilichotokea Arusha, kama nchi ,tumeshindwa. Jumuiya ya Kimataifa inatushangaa,siye tuliopigiwa mfano sasa tunafanana na tunaanza kuachwa na hao walioambiwa waige mfano wetu.
Katika nchi zetu hizi mvunja nchi si mwananchi, bali ni mwanasiasa. Ni kwa kutanguliza mbele maslahi ya kisiasa badala ya kitaifa.
Kule Arusha tumewasikia Dr Slaa na Ndesamburo (CHADEMA) wakitoa kauli za kuchochea hamasa za wafuasi wao. Walipaswa, wakiwa majukwaani, kuwa makini zaidi katika kuchagua na kuchambua kauli zao.
Na kule Arusha tumewasikia pia akina Makamba na Chatanda ( CCM). Walipaswa pia kuchagua na kuchambua kwa makini kauli zao. Kwa kilichotokea Arusha si CHADEMA inayojitafutia umaarufu, bali ni CCM inayoipa umaarufu CHADEMA.
Ni kwa maamuzi kama yale ya kuzuia maandaamano na kauli kama zile za akina Makamba na Chatanda ndizo zinazoisaidia CHADEMA kupanda chati kitaifa na hata Kimataifa.
Na hakika, ni CCM itakayoifanya amani ya nchi yetu ishamiri. Na ni CCM hiyo hiyo itakayoifanya amani ya nchi yetu iporomoke. Nimepata kuandika, kuwa CCM, baada ya uchaguzi wa mwaka huu, ina jukumu la kuongoza mchakato wa mabadiliko ilikiwamo mabadiliko makubwa ya Katiba.
Ukiangalia kilichotokea Arusha, unayaona mapungufu ya Kikatiba yaliyopelekea utaratibu na usimamizi wa uchaguzi wa Umeya ujengeke katika mazingira ya kutoaminiana na hatimaye maandamano na polisi kuingia kwenye vurugu na waandamanaji.
Dalili za kuwepo kwa sintofahamu na vurugu zilionekana mapema. Edward Lowassa, pamoja na yote tunayomwandika, lakini, katika hili la Arusha ndiye mwanasiasa, kwa mtazamo wangu, aliyeonyesha na anayeendelea kuonyesha ukomavu wa hali ya juu katika kipindi hiki cha malumbano ya kisiasa. Kwa la Arusha, Lowassa ameonyesha uwezo wa kusoma alama za nyakati.
Lowassa aliona kile ambacho kingetokea. Akasema hadharani: Kuwa Arusha inaelekea kuwa Ivory Coast, pande zinazohusika zimalize tofauti zao kwa mazungumzo. Ndani ya chama chake kuna waliombeza.Sikushangaa.
Kwa kuhitimisha. Watanzania tutambue ukweli, kuwa demokrasia yetu bado changa. Tumefanya chaguzi zenye walakini mwingi, ni sehemu ya kujifunza. Na sasa tuna fursa ya kuandaa Katiba itakayotufanya tujenge misingi imara ya demokrasia yetu.
CHADEMA iukubali ukweli, kuwa Uchaguzi uliopita umeshapita. Kwamba Serikali iliyo madarakani kwa sasa ndio hiyo inayoongozwa na JK kama Rais. Hatuna Rais mwingine. Hatuna Serikali nyingine.
Na CCM nayo iukubali ukweli, kuwa wakati umebadilika na kuwa wananchi wanaukubali upinzani. Na kwamba kwa sasa, CHADEMA ndio chama kikuu cha upinzani kikifuatiwa na CUF. Vyama hivi na vingine vyenye uwakilishi bungeni, vina lazima ya kushirikiana katika mambo ya msingi na yenye maslahi kwa taifa letu.
Hizi si zama za Mazungumzumzo Baada Ya Habari, bali, Mazungumzo Kabla na Baada Ya Habari, kwa kutanguliza maslahi ya nchi tuliyozaliwa.
No comments:
Post a Comment