Na Lazaro Laurent Memba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na January Makamba, nusu wazichape.
Sugu anayewakilisha Jimbo la Mbeya Mjini (CHADEMA) na January ambaye ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), walitibuana Alhamisi iliyopita kwenye Jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa chanzo kisicho na shaka, wawili hao walikuwa nyuzi chache kuvaana baada ya kukumbushia sakata la dili la Malaria na Sugu kumtuhumu January kwamba alimhujumu.
Chanzo chetu kilisema, January aliomba kuzungumza na Sugu lakini baada ya muda wakaanza kutupiana maneno na kusababisha watu wawazunguke kuwashangaa.
“Sugu alikuwa anazungumza na wabunge wenzake lakini January akaomba wakutane faragha,” kilisema chanzo chetu.
Kilifafanua kuwa kabla ya kuitwa na January, Sugu alikuwa anazungumza na wabunge wenzake wa tiketi ya CHADEMA, Ezekia Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Regia Mtema (Viti Maalumu) na wengineo.
NI DILI LA MALARIA
Chanzo chetu kilimimina ‘data’ kwamba wabunge hao wapya walipokutana faragha, January alimtuhumu Sugu kwa kumchafua kwenye vyombo vya habari.
“January alikuwa anajaribu kumwambia Sugu kwamba yeye hakuhusika na hujuma zozote za kumpora dili la Malaria kama ambavyo imekuwa ikivumishwa.
“Nadhani Sugu hakuelewa utetezi huo, kwa hiyo alimjibu wazi wazi kwamba anajua ukweli na January anahusika, hapo wakaanza kurushiana maneno.
“Sura zao zilionesha wazi kwamba wamekasirika. Alitokea mwandishi wa habari akataka kuwapiga picha wakiwa kwenye hali hiyo, Sugu alikataa katakata.
“Hapo January akaomba japo Sugu akubali wapige picha lakini Sugu akakataa, akasema hata siku moja hawezi kuwa mnafiki kupiga naye picha, ilikuwa tifu kweli kweli,” alisema ‘sosi’ wetu.
Chanzo chetu kilisema kuwa baadaye January naye alikasirika, kwa hilo alimwambia Sugu kwamba akiweza aende Kariakoo akaitishe mkutano aeleze waziwazi malalamiko dhidi yake ili kila mtu ajue.
Kilisema: “Hapo Sugu akawa mkali zaidi, alimueleza January kuwa hawezi kwenda Kariakoo, badala yake atakwenda Bumbuli kumuwashia moto.”
Chanzo chetu kiliongeza kuwa wakati ‘wakiwakiana’, hoja kuu ambayo Sugu aliijenga kwa January ni kwamba wakati akiwa Msaidizi wa Rais, alimzunguka ‘dili’ hilo la Malaria.
Kilisema, Sugu alidai kuwa January ndiye aliyegeuza programu nzima ya mkakati wa kudhibiti Malaria kwa kuitoa mikononi mwake na kumpa mtu mwingine.
KAULI YA JANUARY
Gazeti hili lilimpigia simu January juzi lakini alipopatikana alisema yupo kwenye kikao, hivyo akaomba atumiwe ujumbe mfupi wa maneno (SMS).
Alipoandikiwa SMS kuhusu tuhuma hizo, alikanusha kurushiana maneno na Sugu kwa sababu anamheshimu ukizingatia ni mwakilishi wa wananchi.
Hata hivyo, alipobanwa kuhusu ukweli wa tukio alijibu: “Kutokuelewana na kuwa na misimamo tofauti ni jambo la kawaida hasa kwa watu wa vyama tofauti.”
ALICHOSEMA SUGU
Kwa upande wa Sugu, naye alianza kukanusha lakini alipobanwa alitiririka kuwa anaamini programu ya kudhibiti Malaria iliporwa mikononi mwake, kwa hiyo hawezi kuwa rafiki na mtu aliyemhujumu.
“Yule mtu aliponiita nilidhani anataka kuniambia jinsi alivyohusika kunihujumu badala yake akataka kuniletea siasa.
“Baadaye alinitisha, nikamshangaa. Yaani mimi najua kwamba amefanya dhambi kubwa kunidhulumu halafu ananitisha wakati najua ubavu hana,” alisema Sugu.
KUHUSU SAKATA LA MALARIA
Malalamiko ya mwanzo kabisa ya Sugu ni kwamba aliandaa mradi wa kudhibiti ugonjwa wa Malaria nchini kisha akautafutia mfadhili ambaye ni taasisi ya Marekani inayoitwa Malaria No More.
Aliendelea kusema, baadaye kampuni hiyo ilifika nchini kufanya ukaguzi kabla ya kumwaga mabilioni ya mradi huo lakini mwakilishi wa Malaria No More alipokaribishwa Ikulu, Dar, haki ya kuratibu ikaondolewa kwa Sugu na kupewa mwingine.
Katika hilo, Sugu anadai fidia kwamba wakati wote wa kuandaa mradi huo mpaka kuingia makubaliano na Malaria No More, alitumia gharama nyingi, kwa hiyo anastahili kulipwa.
No comments:
Post a Comment