Katika kile kinachoonekana ni kuumizwa na kitendo cha aliyekuwa mchumba wake, marehemu Perfect Kagisa ‘P.Diddy’ kukaa kwenye uchumba kwa muda mrefu bila kuolewa, Mtangazaji wa Televisheni ya Taifa, TBC1, Maimatha Jesse ‘Mai’ ameonesha kushtuka na kueleza kuwa, hataki hali hiyo ijirudie.
Akizungumza na Risasi Jumamosi juzikati jijini Dar es Salaam, Mai alisema kuwa kipindi kile alifikiri kukaa muda mrefu kwenye uchumba kungeimarisha penzi lao lakini hali ikawa tofauti, hivyo amejifunza kitu.
“Nimekoma kurefusha kipindi cha uchumba kwani hakuna faida zaidi ya kuchokana na kila mmoja kumuona mwezake siyo kitu. Awali nilijua kukaa muda mrefu kwenye hali hiyo kungenogesha penzi kumbe sivyo, nimejifunza vitu vingi kupitia marehemu P.Diddy,” alisema Mai.
Aidha, ili kuondokana na hali ya kuumizwa katika mapenzi, Mai ametaja sifa za mwanaume ambaye anataka awe mumewe wa kudumu na kudai kuwa, asipompata mwenye vigezo hivyo ni bora aishi ‘bachela’.
Alizitaja sifa za mwanaume anayemhitaji kuwa awe mwaminifu ndani ya ndoa, aijali familia yake, awe na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kimaisha, asiwe na wivu kupitiliza, mwenye kuithamini kazi yake, anayemheshimu, asiye mwepesi wa kumnasa vibao anapokosea na mwenye kusamehe wanapokoseana.
No comments:
Post a Comment