Jan 14, 2011

Lulu: Nikila wali njegere lazima nijilambe!

Wiki hii tumehamia kwenye fani ya urembo ambapo tunakutana na mwanadada aliyetokea kung’ara kwenye mashindano ya Miss Sinza 2009 kabla ya kujinyakulia taji la Miss Kinondoni mwaka huo.
Huyu si mwingine bali ni Lulu Ibrahim. Ili kupata mengi zaidi ambayo huenda ulikuwa huyajui kuhusu mlimbwende huyu, ungana nani sasa katika maswali 10 ya moto ambayo nilimbana nayo, naye akanijibu ipasavyo.

TQ: Hebu waeleze wadau wa safu hii kuhusu fani hii ya urembo ambayo kwa sasa ndiyo unayoitumikia. Namaanisha, ilikuwaje mpaka ukajiingiza huku na si kwenye kazi ya saluni au nyingineyo?

LULU: ‘In short’ naweza kusema kuwa, tangu nilipokuwa mdogo nilipenda sana mambo ya urembo ila kilichoniongezea mori ni baada ya kuombwa kushiriki kwa mara ya kwanza nilipokuwa shule ya msingi nchini Kenya. Niliamua kushiriki na kunyakua nafasi ya pili. Huko ndiko safari yangu ya masuala ya urembo ilikoanzia hadi kufikia hatua ya kuvishwa taji la Miss Kinondoni mwaka 2009.
TQ:Baada ya kushindwa hata kufika kumi bora katika mashindano ya Miss Tanzania mwaka huo ulijisikiaje?

Lulu: Nilijisikia vibaya sana hasa baada ya kumalizika kutajwa kumi bora bila jina langu kusikika. Hata hivyo, baadaye niliona kwamba sikuwa na sababu ya kuumia kwani yale ni mashindano kama mashindano mengine hivyo nikakubali kushindwa.
TQ: Tuachane na masuala hayo ya ulimbwende, turudi kwenye maisha yako ya kimapenzi, vipi umeolewa wewe?

LULU: Ai jamani, sijaolewa bado na wala sina mpango wa kuolewa leo au kesho kwani nina mpango wa kujiendeleza kimasomo kwanza.
TQ: Unataka kuniambia ukiwa chuoni hutakiwi kuwa na mume? Au una ‘aleji’ na wanaume?

LULU: Duh! We’ naye na maswali yako, inaruhusiwa ila kwa sasa bado najiandalia maisha ya baadaye zaidi ingawa najua ipo siku nitalazimika kuingia katika maisha ya ndoa, wakati ukifika tutapeana taarifa.
TQ: Ukifanikiwa kuingia katika maisha ya ndoa, ungependa kupata watoto wangapi na wa jinsia gani ?

Lulu:Siku zote huwa natamani kuwa na familia ya watoto wawili tu tena wa kike na wa kiume, ikiwa hivyo ndoto zangu zitakuwa zimetimia na nitafurahi sana.
TQ:Ni mwanaume wa aina gani ambaye ungependa awe mumeo?

Lulu: Mwenye kujiamini, aliyeelimika na mwenye uwezo wa kunisaidia katika maisha yangu.
TQ: Warembo wengi wamekuwa wakilalamikiwa juu ya masuala ya ushirikina wawapo kambini na wengine kutumia vilevi kabla ya kupanda stejini je, kwa upande wako unalizungumziaje hilo?

LULU:Mimi sijawahi kukumbana na ishu kama hizo ingawa nilishawahi kusikia baadhi ya watu wakisema.
TQ:Vipi kuhusu skendo za ufuska kwa mamiss, wapo warembo kama akina Wema Sepetu, Miriamu Gerald na wengineo ambao wameichafua fani hii ya urembo, nini wito wako kwa warembo wenzako?

LULU: Ninachoammi ni kwamba si kila anayeshiriki mashindano haya ana tabia chafu, wapo wastaarabu ila nawaomba wale wenye tabia kama hizo kuacha mara moja kwani haileti picha nzuri kwenye jamii.
TQ:Unavyoonekana ni mtu wa kujirusha sana, ni viwanja gani ambavyo hupenda kwenda ?

LULU: Mara nyingi ‘outing’ zangu huwa ni Beach nikiwa na marafiki zangu na siku moja moja napenda kwenda kumbi mbalimbali za burudani.
TQ :Tutajie vitu ambavyo unavipenda sana katika maisha yako.
LULU:Kwa upande wa chakula, nikila wali njegere lazima nijilambe, rangi nyeupe, nyekundu, nyeusi na bluu ndiyo chaguo langu na gari napenda Toyota special rangi nyeusi.

No comments: