Jul 10, 2013

"VYOMBO VYA HABARI HUWA VINAHONGWA NA WAPINZANI ILI VIWAANDIKE VIZURI".....SPIKA WA BUNGE



Spika wa Bunge, Anne Makinda, ameibuka na kauli yenye utata mkubwa akivituhumu vyombo vya habari kwamba vinahongwa na wabunge wa kambi ya upinzani ili viandike habari zao vizuri.

Bila kufafanua ni kwa jinsi gani wabunge hao wanatoa hongo hiyo mbali tu ya kusema wanatoa kitu kidogo ili waandikwe vizuri, pia alikana kuwakandamiza wabunge wa kambi hiyo na kuwabeba wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wako upande wa serikali.

Alisema hana upendeleo katika uendeshaji wa vikao vya Bunge kama anavyoshambuliwa na baadhi ya watu na kwamba lawama zinazoelekezwa kwake zinatokana na watu kuangalia upande mmoja.

Spika Makinda alitoa ufafanuzi huo jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu vurugu mbalimbali zinazotokea katika vikao vya Bunge mjini Dodoma na hasa juu ya kuporwa au kugeuzwa kwa hoja za upinzani.

Spika Makinda alikuwa ametoka kuzungumza na Spika wa Korea Kusini, Kang Chang Hee.

"Ndiyo najua mnapewa 'kitu kidogo' na hawa wanaoanzisha vurugu bungeni, lakini kusema Spika anapendelea hili siyo kweli hata kidogo,"
aliongeza Spika.

Alisema iwapo angekuwa na kawaida ya kuwakandamiza wabunge wa upinzani kwa kiasi kinachosemwa wengi wa wabunge hao wa upinzani wasingekuwapo bungeni.

“Mimi siwapendelei wabunge wa CCM, ningekuwa hivyo hawa wapinzani wasingekuwapo bungeni,” alisema Makinda muda mfupi baada ya kuzungumza na ujumbe wa Bunge la Korea Kusini uliomtembelea ofisini kwake.

Makinda alisema wakati wa kuendesha vikao vya Bunge haitakiwi kuwa na itikadi za vyama na kwamba kufanya hivyo kunaweza kusababisha vurugu.

Wakati Spika akitoa utetezi huo, wabunge wa upinzani kwa nyakati tofauti wamekuwa wakimtupia lawama za wazi hususani wanapokuwa katika vikao vya Bunge kwamba anawapendelea wabunge wa CCM.

Miongoni mwa mambo ambayo Spika Makinda amekuwa akilaumiwa ni pamoja na kukalia zaidi ya taarifa 10 za ushahidi juu ya kauli za wabunge wa upinzani zilizowasilishwa kwake na yeye kuzikalia kwa muda wote bila kusema lolote.

Miongoni mwa ushahidi huo, umo wa mawaziri kusema uongo bungeni.

Pia Spika amekuwa akilaumiwa jinsi mjadala wa hoja binafsi za wabunge wa upinzani ‘zilivyoporwa’ na serikali, kama ile ya Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, kuhusu mitalaa ya elimu; ya mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika jiji la Dar es Salaam, na hata ya Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, kuhusu ardhi ya Meru.

Zote hizi ama ziligeuzwa na kupoteza maana yake hali iliyosababisha mvutano mkali bungeni ukiacha picha ya upendeleo wa dhahiri kwa baadhi wafuatiliaji wa mijadala ya Bunge.

Akizungumzia mchakato wa kupata Katiba mpya, Spika Makinda alisema Bunge la Katiba litakutana Novemba, mwaka huu na  litawajumuisha wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na wajumbe 160 ambao hata hivyo alisema sheria haijasema wanapatikana vipi.

Alisema mwezi ujao serikali inatarajia kupeleka muswada wa sheria ili kufanya marekebisho ya namna ya kupata wajumbe hao 160 ambao siyo wabunge.

Spika alisema katika Bunge hilo, yeye hatakuwa mwenyekiti na kwamba wajumbe wenyewe watachagua kiongozi atakayewaongoza.

Kauli ya Makinda iliwahi kusemwa pia na Naibu wake, Job Ndugai, mara baada ya kuahirisha kikao cha Bunge kwenye mkutano uliopita, kufuatia vurugu zilizotokea baada ya hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani Wizara ya Mambo ya Nje, Ezekiah Wenje, kutamka kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kina uhusiano na vyama vinavyounga mkono mashoga.

Wakati vurugu zikiendelea nje ya viwanja vya Bunge kwa wabunge wa CUF na Chadema kuzozana, Ndugai alipita ndipo aliulizwa na waandishi Kulikoni, lakini katika hali ya kushangaza, alivituhumu vyombo vya habari kwamba ndivyo vimesababisha hali hiyo.

“Haya yote mmesababisha ninyi waandishi, mnawadekeza sana wabunge wa upinzani, hata wangefanya nini mnawapamba pamba, lakini mkumbuke siku wakiingia madarakani watafanya haya haya wanayofanya leo,” alisema Ndugai bila kufafanua kauli yake.

Kwenye mazungumzo yake na ujumbe wa Bunge la Korea uliomtembelea ofisini kwake, Spika alisema unalenga kudumisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali zikiwamo za uwekezaji na kuendeleza uchumi wa nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Spika wa Korea, Chang Hee alisema nchi yake imepiga hatua kubwa ya maendeleo ingawa haina chanzo chochote cha kuzalisha nishati ya umeme ikilinganishwa na Tanzania.

Alisema Bunge la Tanzania linafanya vizuri kwa upande wa nafasi za viti maalum ikilinganishwa na Korea Kusini ambayo idadi ya wanawake bungeni ni ndogo.

No comments: