Jul 10, 2013

"NITAENDELEA KUPAMBANA NA WABISHI WASIOTAKA KUHAMA ILI KUPISHA MIRADI YA UJENZI"...MAGUFULI



WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli ameapa kupambana kwa kuwabomolea au kuwakomesha kwa njia nyingine, watu waliogoma kuhama kwa ajili ya kupisha miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na wizara yake.

Katika hilo, tayari amekwishatangaza uamuzi mzito wa kuruhusu kampuni ya ujenzi ya Jaspal Singh, kujenga barabara kwa kiwango cha lami kwa kuzizunguka nyumba za wakazi waliogoma kuhama na kukimbilia mahakamani akiamini kuwa wataondolewa kwa kugongwa na malori yatakayokuwa yakipita baada ya barabara hiyo kukamilika.

Pamoja na hilo, Dk. Magufuli amesema atazibomoa bila kulipa fidia nyumba za wananchi nane waliokataa kufanyiwa tathmini ili kupisha mradi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni, endapo hawatabadili msimamo wao huo.

Uamuzi huo aliutangaza jana baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam, ambapo alibaini kuwa miradi mingi inakwamishwa na wananchi wa maeneo husika.

Akiwa katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Kigogo hadi Jangwani yenye kilomita 2.7, alishangazwa kuona mradi umesimama huku vifaa vikionekana kuwa na kutu kitendo ambacho kilimlazimisha ahoji.

Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Mussa Ali pamoja na Mkandarasi Jaspal Hungh, walimueleza Magufuli kwamba kuna wananchi wenye nyumba 16 wamechukua fidia na kufungua kesi mahakamani kwa kudai kiasi walichopewa ni kidogo.

Aliongeza kuwa kesi hiyo imechukua zaidi ya miaka miwili bila kutolewa hukumu na kusababisha mradi kukwama.

TAMKO LA KIGOGO

Akizungumzia hilo Magufuli alisema: “Naomba tusiingilie mahakama lakini naagiza kuanzia leo (jana), anzeni kujenga barabara ya lami kwa kuzizungushia lami nyumba hizo na kuruhusu gari zipite, nadhani haitapita wiki kabla hazijagongwa na malori ya mchanga, sitaki kusikia Serikali inadaiwa fidia ya ucheleweshaji wa mradi.

“Pia naagiza kwamba mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki kwamba meneja wa mradi fungua kesi dhidi ya wananchi hao waliochukua fedha za fidia na kwenda mahakamani, huo ni wizi.

“Serikali ikishinda kesi ya madai yao ya fidia ndogo, wao ndio watawajibika kujenga sehemu ya nyumba zao, hatuwezi kuchezea fedha kwani kuwafidia Sh bilioni 3.8 ambapo mradi wenyewe unagharimu Sh bilioni 7.6.

“Kuna mazoea yameibuka ya watu kuchezea Serikali na mahakama, sasa nasema katika miradi ya wizara yangu nitapambana nao watu wenye kiburi cha kuchezea vyombo hivyo,” alisema.

DARAJA L A KIGAMBONI

Awali akitembelea eneo la Kigamboni uliko mradi wa daraja la Kigamboni, Magufuli aliwataka wananchi nane waliokataa kufanyiwa tathmini ya nyumba zao ili kupisha mradi huo, kubadili msimamo wao haraka kabla ya Serikali haijazibomoa nyumba hizo kwa nguvu tena bila kulipwa.

Jumla ya watu 121 walitakiwa kuhama kupisha mradi huo ambapo kati yao 113 walikubali kufanyiwa tathmini na kulipwa jumla ya Sh bilioni 11.7, lakini nane walikataa.

“Nasema Serikali ikiamua kufanya ukorofi utakuwa mkubwa kuliko msimamo wako, sasa nasema hao waliokataa kufidiwa naomba wasiambulie patupu kabla hatua hazijachukuliwa, wakubali kuchukua kiasi kitakachothaminiwa haraka, sisi tukija tutabomoa na hatukulipi na mradi utaendelea.

“Naomba daraja hili likamilike na kukabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete Januari 31, 2015 na kulifungua, sitaki kuona linafunguliwa na rais mwingine ambaye anaweza kusema yeye ndiye aliyejenga wakati ni uongo, aliyeweka jiwe la msingi ndiye atakayefungua,” alisema.

Mradi wa daraja la Kigamboni unagharimu Sh bilioni 214 na kati hizo asilimia 40 zinatolewa na Serikali wakati Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), unachangia asilimia 60.

Mbali na hilo, Dk. Magufuli ameagiza kuondolewa haraka wakazi wa eneo la Davis Corner, Temeke ambao licha ya kulipwa fidia ili kupisha ujenzi wa barabara ya Jet Corner hadi Temeke, wameshindwa kuhama mpaka sasa na badala yake kutumia fedha hizo kuendeleza ujenzi na kudai malipo mengine.

Magufuli alishangazwa kuona wananchi hao ambao wamegoma hadi sasa wamelipwa fidia Sh 15.8 huku mradi wenyewe ukiwa Sh bilioni 12 na barabara ikiwa haijakamilika.

Mradi wa mabasi ya kasi

Akikagua mradi wa mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam (DARTS), Magufuli alifurahishwa na kasi pamoja na kiwango cha ujenzi wa mradi huo, ambao utapunguza msongamano wa magari.

Meneja wa mradi wa Darts, Baraka Ally alimweleza Dk. Magufuli kwamba mradi unaendelea vizuri na utakamilika kwa wakati uliopangwa.

Hata hivyo alisema changamoto kubwa inayoukabili mradi huo ni uvamizi wa wafanyabishara ambao wamekuwa wakiweka biashara zao barabarani huku wenye teksi na magari mengine wakiegesha eneo la mradi.

Vile vile alisema kuwa kuna hatari kubwa ya Jiji la Dar es Salaam kukumbwa na harufu kali kutokana na wakazi wanaoishi karibu na barabara kujiunganishia kinyemela mabomba ya maji machafu na mifereji ya mvua.

Magufuli aliagiza watu wote wanaokwamisha mradi huo kuchukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na halmashauri kuwajibika katika hilo.


MTANZANIA

No comments: