Wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, UNBOA wakiwa katika picha ya pamoja na Msimamizi Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi Susan Malcora mara baada ya ya Tanzania na Afrika ya Kusini kuachiana kijiti. Tanzania ilipitishwa kwa kauli moja na Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa katika mkutano wake uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, kuwa mjumbe wa Bodi ya UNBOA ambapo itafanya kazi na wajumbe wengine wawili ambao ni China na Uingereza |
Naibu Mkaguzi Mkuu kutoka Afrika ya Kusini Bw. Thembele Makwetu akimkabidhi mkoba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh,ikiwa ni ishara rasmi ya Ofisi yake kuingia katika Ujumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa. Mdhibiti na Mkaguzi na Ofisi yake anachukua nafasi inayoachwa wazi na Afrika ya Kusini ambayo imekuwa mjumbe wa Bodi hiyo kwa miaka 12. Tanzania kupitia Ofisi ya Mdhibiti Mkuu itashika nafasi hiyo kwa miaka sita. Wanaopiga makofi kutoka kushoto ni Mkaguzi Mkuu kutoka Uingereza Bw. Amyas Morse ambaye naye ni mjumbe wa Bodi na Bw. Dong Dasheng jumbe wa Bodi pia na ni Naibu Mkaguzi Mkuu kutoka China. |
Ilikuwa ni furaha tupu kwa Wakaguzi hawa wawili baada ya kukabidhiana majukumu. Afrika ya Kusini ambayo ndiyo imemaliza muda wake wa Ujumbe katika Bodi hiyo, imetoa ushirikiano mkubwa kwa timu ya Tanzania katika kipindi chote tangu Tanzania ilipopitishwa kuwa Mjumbe wa Bodi hiyo mwishoni mwa mwaka jana. Maafisa kutoka ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wamefanya kazi bega kwa bega na maafisa wenzao kutoka Afrika ya Kusini, ushirikiano ambao umewezesha mchakato mzima kuelekea makabidhiano kufanyika kwa ufanisi mkubwa sana. |
Mhe.Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza wakati wa makabidhiano hayo ambapo aliiwakilisha Serikali, Balozi Sefue wakati huo akiwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa, alitoa mchango Mkubwa katika kuhakikisha kwamba Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali inapata nafasi hiyo. akizungumza katika makabidhiano hayo aliwahakikishia wajumbe wa Bodi hiyo kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaichukulia nafasi ya hiyo ya kuwa mjumbe wa kukagua mahesabu na mali za Umoja wa Mataifa kwa uzito wa hali ya juu sana. |
Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh akizungumza wakati wa makabidhiano hayo. Ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza sana suala la kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote bila ya upendeleo, au kukomoana na kwamba Tanzania imejipaga vema kulibeba jukumu hilo kwa hali na mal na kwamba uwezo pia inao. |
Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika makabidhiano hayo. Kutoka kushoto ni Bibi Magdalena Rweyemamu, Bw. Francis Kitauli, Bw. Edwin Rweyemamu anayeteta jambo na Bw. Ludovick Utouh, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Bw. Salhina Mkumba na Bw. Athanas Pius.
=====
Na Mwandishi Maalum
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekabidhiwa rasmi Ujumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa ( UNBOA)
Makabidhiano hayo yamefanyika siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa mkutano wa 66 wa Bodi ya Wakaguzi ya UM.
Katika hafla hiyo Afrika ya Kusini ndiyo iliyoikabidhi Tanzania kijiti hicho. Makabidhiano ambayo yalishuhudiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Ombeni Sefue ambaye ameiwakilisha Serikali katika makabidhiano hayo.
Afrika ya Kusini imekuwa mjumbe wa Bodi kwa miaka 12 na Tanzania itamaliza ngwe yake mwaka 2018
Aidha hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Bi Suzan Malcora ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (Chief de Cabinet). Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki Moon.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyowashirikisha pia wajumbe wengine wa bodi ambao ni Bw. Dong Dasheng akimwakilishi Mkaguzi Mkuu kutoka Uchina na Bw. Amyas Morse Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Uingereza. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu , Bw. Ludovick Utouh amewahakikisha wajumbe wenzie pamoja na sekretariati ya Umoja wa Mataifa kwamba Ofisi yake imejipanga vema kulibeba jukumu hilo.
“ Hafla hii ya leo inahitimisha rasmi mchakato mrefu wa makabidhiano ya jukumu hili, mchakato ulioanza tangu uteuzi wangu ulipofanyika mwezi Novemba mwaka jana. Ni mchakato unaofungua ukurasa wa kubadilishana mawazo, uzoefu na utaalamu. Kwa niaba ya Nchi yangu, Ofisi yangu na mimi mwenyewe binafsi naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa wajumbe wa Bodi ya UM na Kamati ya Operesheni za Ukaguzi” akasema Bw. Otouh.
Akabainisha kwamba Tanzania inachukua jukumu hilo la kuwa mjumbe wa UNBOA katika kipindi muhimu, kipindi ambacho UM unapita katika mageuzi makubwa ya kubadili mifumo yake ya kiutendaji ikiwamo kutoka utumiaji wa mfumo ujulikanao kama UNSAS kwenda mfumo wa IPSAS.
“ Tunaingia katika bodi hii katika kipindi ambacho UM inapitia mageuzi makubwa yakiwamo yale ya kutoka ukaguzi uliokuwa ukifanyika kila baada ya miaka miwili na kuingia katika ukaguzi wa kila mwaka”. Akasisitiza Otuoh
Na kuongeza. “ Matokeo ya mageuzi haya maana yake ni kuongezeka kwa ukubwa wa kazi kwa upande wa wakaguzi, ogezeko ambalo litatupasa si tu kufanya kazi kwa umakini mkubwa lakini pia kutekeleza majukumu mengi na katika muda mfupi”.
Na kwa sababu hiyo, akasema, kwa kutambua uzito na unyeti wa kazi kubwa iliyombele, ndiyo maana baada ya kuteuliwa kwake yeye na maafisa wake walianza jukumu la kujianda kwa kila hali ili waweze kulitekeleza jukumu hilo kwa ukamilifu na weledi mkubwa.
Akatumia fursa hiyo kuishukuru Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Afrika ya Kusini kwa namna ambavyo imetoa ushiriano mkubwa na wa karibu sana, kuanzia siku ile Ofisi ya NAOT ilipopitishwa kwa kauli moja na Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa kushika wadhifa huo.
Aidha akasema ingawa Afrika ya Kusini imemaliza ujumbe wake, Tanzania itaendelea kushirikiana nayo kwa karibu hasa kwa kuzingatia kwamba kukabidhiwa kwa jukumu hilo hakuhitimishi mchakato mzima wa kuendelea kubadilishana uzoefu na utaalamu.
Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza kwa niaba ya serikali, pamoja na kuwashukuru wajumbe wa bodi ya UNBOA na sekretarieti yake. Amesema Serikali inauchukulia ujumbe huo kwa uzito wa aina yake.
“Nimefurahi sana kuwapo hapa na kuiwakilisha serikali, ninapenda ninawakikishie kwamba, serikali yangu inalipa jambo hilo uzito wa kipekee sana. Heshima na mchango wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa unafamika na sasa tunapoingia katika jukumu hili ni dhahiri kwamba tunataka kufanya kazi nzuri hata katika maeneo mengine na uwezo huo tunao” akasisitiza.
Naye Naibu Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu kutoka Afrika ya Kusini Bw. Thembekile Makwetu akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, amemhakikisha Bw. Utouh na ofisi yake ushirikiano wa karibu na usiotereka. Huku wajumbe wengine wa Bodi nao wakielezea kutoa ushirikiano kwa Tanzani na kuikaribisha kwa moyo mkunjufu.
Kwa upande wake, Bi Susan Malcora akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, yeye amesema anaikaribisha Tanzania katika ujumbe wa bodi hiyo kwa mikono miwili na kusisitiza kwamba ujumbe wa Tanzania katika Bodi hiyo utasaidi sana katika kusukuma mbele ajenda ya uwajibikaji na udhibiti wa fedha na mali zinazomilikiwa na Umoja wa Mataifa.
SOURCE: mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment