Mahakama kuu kanda ya Dodoma imetupilia mbali ombi la wanachama wawili wa CCM waliofungua kesi ya kupinga matokeo ya ubunge ambayo yalimpa ushindi mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kupitia CHADEMA mwaka 2010.
Jaji Moses Mzuna amesema watoa hoja katika kesi hiyo wameshindwa kuthibitisha hoja zao 11 walizomtuhumu mbunge huyo, msimamizi wa uchaguzi na mwanasheria wa serikali, ambapo baada ya mashahidi 24 wa wadai kutoa ushahidi na wengine wanne wa wadaiwa, Jaji amesema ameona uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki na ulifuata taratibu zote.
Hata hivyo Lissu alishindwa kujizuia na kutokwa na machozi kutokana na matokeo ya shauri hilo ambalo lilisikilizwa mfululizo kuanzia March 12 2012 ambapo wadai walikua ni Shaban Selema Itambu na Paschal Masele Hallu wakazi wa kijiji cha Makiungu Singida Vijijini waliotetewa na wakili Godfrey Wasonga wa Dodoma.
Baada ya kutangazwa huru, Lissu amesema “kesi ilikua ya mambo ya kutunga uongo, mambo ya kuhakikisha sifanyi mambo ya wananchi lakini leo Mahakama imethibitisha kile ambacho nilisema siku zote, haki imetendeka na tuhuma zote walizozileta hakuna hata moja iliyothibitishwa, nawashukuru sana wananchi waliokua pamoja na mimi kwa miezi miwili yote hiyo ambayo tumeshinda tunapotezewa muda hapa”
No comments:
Post a Comment