Tumshukuru Mungu kwa kutupa uhai leo huku tukimuomba aziweke roho zao mahali pema peponi waliokufa kwa mabomu wiki iliyopita huko Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Tunaamini wote waliokufa ambao tulikuwa tukiwapenda sana, Mungu amewapenda zaidi.
Baada ya kusema hayo, sasa tukumbushane tu kwamba katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tunalolitegemea kwa ulinzi wetu, kumekuwa na matukio mengi ambayo yanapaswa kuitwa ni majanga.
Ndugu zangu, mtu mwenye kufikiri ni lazima ajiulize, nini kinasababisha haya majanga kutokea ndani ya jeshi hili mara kwa mara?
Wakati baadhi ya watu waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wameanza harakati za mazishi ya wapendwa wao ambao walipatwa na janga la milipuko hiyo ya mabomu ya jeshi katika kikosi cha 511, tutafakari kwa pamoja matukio yafuatayo kisha tuchekeche ubongo kuona nani wa kulaumiwa.
Ndugu zangu, kweli inawezekana hizi ajali ni za bahati mbaya lakini kinachosumbua wananchi wengi hasa wenye uwezo wa kutafakari na kujenga hoja kwa kutazama mwenendo wa mambo ndani ya nchi yao, ni kujirudia kwa tukio hili la kulipuliwa watu na mali zao kwa kipindi kifupi sana.
Ndugu zangu, hebu tuangalie matukio ndani ya jeshi letu, tukianzia na Desemba 2007 ambapo helikopta ya kijeshi ilianguka kwenye Ziwa Natron.
Katika ajali hiyo, ndani ya helikopta kulikuwa na watalii wanne na maofisa watatu wa jeshi la wananchi lakini mwaka uliofuatia, yaani Juni 2008 helikopta ya pili ilianguka Oljoro, Arusha wakati ikianza safari ya kwenda Dar es Salaam. Watu wote sita waliokuwemo ndani walipoteza maisha wakiwemo watoto wawili.
Lakini janga lingine linalofanana na hili la Gongo la Mboto ni lile la Aprili, 2009 na Septemba 2009 katika kambi ya jeshi 671 KJ Mbagala Kizuiani, ambako ghala la silaha lililipuka mabomu.
Hakika ndugu zangu wengi tunakumbuka kuwa maafa yalikuwa ni makubwa mno, kwani watu zaidi ya 25 walikufa na majeuri walikuwa ni mamia. Tulisikia viongozi wetu wakituambia kuwa tukio kama hilo halitatokea tena.
Mwaka jana, Juni 2010 ajali ingine ikatokea, ndege ya JWTZ kutoka Ngerengere ilipoanguka katika Kijiji cha Manga, mpakani mwa Mikoa wa Tanga na Pwani, wilayani Handeni. Katika ajali hiyo marubani wote wawili walikufa.
Katika ajali hiyo tuliambiwa ndege hiyo iligonga lori lililokuwa na watalii na kusababisha lipinduke, hakika madhara kwa watalii yalikuwa makubwa.
Ndugu zangu, kumbukumbu zinaonesha kwamba mwaka 2005 kulitokea mlipuko kama huu katika Kikosi cha Jeshi Gongo la Mboto. kwa bahati nzuri tukio hilo halikuleta maafa kwa wananchi na mali zao na halikutangazwa sana.
Mbaya zaidi ni kuwa kila majanga haya yanapotokea umma huwa haupatiwi taarifa ya ripoti ya uchunguzi kwa kisingizo kimoja tu kuwa taarifa hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya kijeshi.
Kwa mtazamo wangu kutokana na madhara kwa raia, ingefaa basi hao wanaoandaa taarifa wakaandaa mbili, moja kwa jeshi na nyingine kwa raia ili waelewe nini kilisababisha waumie na bila shaka itaeleza mbinu ya kujikinga na mabomu pindi hali kama hiyo inapotokea.
Kufanya hivyo kutapunguza au kufundisha raia mbinu ya kuepuka madhara kama hayo siku za usoni.
Ndugu zangu, mbaya zaidi ni kuwa katika mtiririko wa matukio tuliyoyaorodhesha, uongozi ama wa kisiasa au kijeshi ni ule ule. Hapo linazuka swali, kama vigogo ni wale wale hawaoni kuwa kuna haja ya kuepusha majanga haya yanayojirudia? Kama jibu ni ndiyo, wafanye nini sasa?
Tatizo la kulipuka mabomu jeshini na kuua raia na kuharibu mali zao na za serikali kujirudia ndiyo kinachowauma watu. Taarifa rasmi za kiserikali zinaeleza kuwa watu 21 wamekufa, 315 kujeruhiwa na wengine takribani 135 kulazwa hospitalini kutokana na milipuko hiyo, hakika inauma sana.
Wote tumesikia taarifa ya Baraza la Taifa la Usalama ambayo inaonesha kwamba hakuna atakayewajibika. Kwa msingi huo kila kitu kinachukuliwa kama bahati mbaya tu; hakuna wa kulaumiwa.
Ndugu zangu, tumesikia serikali ikisema kwamba baada ya janga hili sasa imeamua kuomba msaada kwa nchi rafiki kusaidia katika uchunguzi wa chanzo cha milipuko na kushauri namna bora zaidi ya kuimarisha usalama na uhifadhi wa silaha za moto katika maghala ya JWTZ.
Ndugu zangu, niwaambie tu wahusika huko jeshini kuwa umma bado umepigwa na bumbuwazi. Hii ni kwa sababu miaka ya nyuma taifa halikuwa na majanga kama haya tofauti na sasa.
Kipindi hicho teknolojia ya kuhifadhi na hata kutengeneza silaha za moto ilikuwa chini tofauti na sasa. Pia jeshi lilikuwa na wanajeshi wasomi wachache zaidi. Kwa nini matatizo kama haya yasitokee kipindi hicho? Tunatanzika zaidi kupata jibu la maana juu ya mfululizo wa majanga yanayotokea sasa.
Tunashindwa kupata jibu la swali kwamba tukio moja halitoshi kutoa fundisho kwa ajili ya kuepuka madhara kama haya siku za usoni? Hakika matukio yanayopoteza roho za watu jeshini yamekuwa mengi kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Viongozi tafakarini hili ili kuepuka janga kubwa zaidi ya hili.
Jipu limepasuka siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
No comments:
Post a Comment