Feb 22, 2011

BM-21: Makombora ya Kirusi yenye kupiga umbali wa kilomita 20

*Hupigwa kutoka kwenye gari maalumNI makombora yenye uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 20.  Yalitengenezwa Urusi tangu mwaka 1963 na hupigwa kutoka kwenye gari maalum linalojulikana kama BM-21 Grad.  Ni gari aina ya Ural-375D.

Gari hilo lina kasi ya juu ya kilomita 75 kwa saa, linaweza kusafiri bila “kupumzika” kwa kilomita 750, na lina uwezo wa kupita sehemu mbalimbali “ngumu”.

BM kwa Kirusi ni “Boyevaya Mashina” maana yake ikiwa ni “gari la kivita” au “gari la mapigano”, na neno “Grad” ambalo ni jina la gari lenyewe lina maana ya “mvua ya mawe”. 

Neno hilo bila shaka linatokana na jinsi mtambo wa kuyafyatua makombora hayo unavyozunguka na kuvuruga eneo kubwa la adui ambapo huwa unabeba makombora 40 yenye kipenyo cha milimita 122.

Shambulio lake la kutisha ni sawa na mvua ya mawe inavyoogopwa!
BM-21 Grad, ni mfumo wa ufyatuaji makombora mengi kwa wakati mmoja, kwa Kiingereza ukijulikana kama “Multiple Rocket Launcher”.
http://www.exchange3d.com/images/uploads/aff4309/Grad/BM21_Grad%203%20(1).jpg
Kwa mujibu wa wataalam wa masuala ya kivita, BM-21 Grad, umedhihirika kuwa bora zaidi duniani kuliko mfumo mwingine wa mashambulizi ya ardhini, na ndiyo maana nchi zingine zimebuni mfumo kama huo ambao ni wa maangamizi makubwa kwa adui kama hakujiweka sawa.

Kwa vile mtambo wa kurusha makombora hayo huzunguka, makombora hayo ni lazima yainuliwe juu (mshazari) ili kukwepa kuibomoa sehemu anayokaa dreva wa lori hilo ambalo lina mitambo maalum miwili ya kulishikilia lisiyumbishwe au kuanguka kutokana na milipuko ya makombora yanayopigwa.

Wakati wa kusafirishwa, makombora hayo huelekezwa mbele kwa juu, na ulipuaji wa makombora unaweza kufanywa kwenye chumba cha dereva wa lori au kwa kutumia mtambo maalum (remote control) kutoka kwa mbali kidogo.

Ni lazima pia pawe na jenereta maalum kwa ajili ya kuhakikisha kuna nguvu za kufanya kazi kwa mtambo huo wa kuyalipua makombora ambayo hujazawa haraka kila yanapomalizika.

Gari hilo linaweza kuyafyatua makombora yote katika sekunde sita, au kuyafyatua kila moja kwa wakati wake!
Mtambo huo unaweza pia kujijaza makombora katika dakika tano tu, na kuyafyatua makombora yote 40 mara moja au baada ya nusu sekunde kila moja.

Vilevile, makombora hayo yanaweza kupigwa kwa mkono inapotakiwa ambapo watu watano wanaohusika katika jukumu hilo wanaweza kuyajaza maroketi hayo kwa kutumia mikono katika dakika nane.
Kwa vile maroketi hayo huathiri eneo kubwa, yanafaa kufanya mashambulizi dhidi ya adui aliye eneo la wazi na kwa kufanya mashambulizi ya silaha za sumu. 

Mlipuko mmoja wa roketi hilo hutoa risasi 720, na kwa vile mtambo huo huzunguka, silaha hizo hazifai kutumiwa  katika eneo ambalo wanaozipiga  wanataka kulifikia likiwa salama.

Hayo ndiyo makombora ya BM-21 ambayo yakilipuka yenyewe, madhara yake hayafiki zaidi ya umbali wa kilomita tano, lakini yakipigwa makusudi kutoka kwenye mtambo wake kwenye lori la “Grad” yana uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 20.

Yakipigwa kutoka jijini Dar es Salaam, yanaweza kufika au kukaribia Kibaha!  Inatisha!

No comments: